JESHI LA POLISI NCHINI LIMEMFUKUZA KAZI ASKARI ALIYEINGIA UKUMBI WA DISCO AKIWA NA BUNDUKI

KAMANDA wa Polisi Kikosi cha Operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu na majambazi, maarufu kama Kimbunga, Simon Sirro, amesema kuwa wamemtimua askari wao aliyeingia ukumbi wa disko mjini Bukoba akiwa na bunduki kwa ajili ya kulipa kisasi.

Sirro alitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari jana wakati akielezea mafanikio waliyoyapata katika operesheni hiyo kwa kuwakamata watuhumiwa 88 wanaojihusisha na ujambazi na biashara ya silaha.
Alimtaja askari huyo kuwa ni mwenye namba H 85, PC Alphonce, aliyekuwa ametokea mkoani Mara kwa ajili ya kushiriki operesheni hiyo mkoani Kagera.

Alisema kuwa PC Alphonce alikorofishana na baadhi ya watu ndani ya ukumbi wa disko, hivyo akatoka nje kufuata bunduki, kisha akarudi nayo kwa ajili ya kuwadhuru ‘wabaya’ wake, lakini askari wenzake waliokuwamo ndani walifanikiwa kumzuia kabla ya kutimiza azima yake.

Kuhusu kukamatwa kwa Mkurugenzi wa redio ya kijamii iliyoko wilayani Karagwe (FADECCO) na kuwekwa ndani siku mbili, kisha kuachiwa kabla ya kukamatwa tena, Sirro alisema uchunguzi unaendelea kubaini uraia wake ambao umeonekana kuwa wa shaka.

Wakati huo huo, watuhumiwa 88 wa unyang’anyi wa kutumia silaha wamekamatwa wakiwamo watano wanaojihusisha na biashara ya uuzaji wa silaha mbalimbali.

Kamanda Sirro alisema kuwa wameweza kuwakamata watuhumiwa wanaojihusisha na biashara ya silaha mbalimbali kutoka nchini Burundi.

Alisema watuhumiwa hao baada ya kuhojiwa, mmoja wao alikiri kuwa alikuwa akifanya biashara ya kuuza mbuzi ambao alikuwa akiwatoa Tanzania na kuwapeleka Burundi, baadaye akashawishiwa kuwa biashara hiyo hailipi, badala yake afanye biashara ya kuuza silaha.

Kamanda Sirro aliongeza kuwa katika mahojiano hayo watuhumiwa walisema kuwa huko Burundi wanazinunua silaha kwa bei rahisi ya sh 100,000 na kuziuza kwa sh milioni 1.5 Tanzania.
Kwa mujibu wa Sirro, majina ya watuhumiwa hao yamehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi ili kuwabaini wanaozinunua huku Tanzania.

Alisema watuhumiwa wawili kazi yao ilikuwa kufuata silaha Burundi na watatu walikuwa wakizisambaza kwa wateja wao hapa nchini, na kwamba watuhumiwa wote 88 ni Watanzania.

“Silaha 23 zimekamatwa zikiwemo SMG tatu, pisto mbili, magobore 18, risasi 484 za SMG/SAR 471, pisto 13, magazine mbili za SMG, bomu moja la kutupwa kwa mkono na sare moja ya jeshi la Burundi,” alisema.
Aliongeza kuwa katika operesheni hiyo pia wamekamata ng’ombe 103 mali ya Kalemera George katika Hifadhi ya pori la Biharamulo, ambao walipelekwa mahakamani kwa kutumia sheria ya wanyamapori, ambako iliamriwa wataifishwe.

Kamanda Sirro alisema kuwa wahamiaji haramu 425 wamekamatwa katika awamu ya pili ya Opersheni Kimbunga, Wanyarwanda wakiwa 149, Warundi 180, Waganda 82 na Wakongo 14.
Wahamiaji 122 waliondoka kwa hiari na 39 waliachiwa huru baada ya mahojiano.

Alisisitiza kuwa operesheni hiyo ni endelevu na haichagui tabaka la mtu, isipokuwa inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kwa kuzingatia haki za binadamu.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima

Comments

  1. Kweli huyo askari hafai katika jamii,inabidi sheria ichukue mkondo wake ili iwe fundisho kwa wengine wenye kutumia madaraka kama mwamvuli,nalipongeza jeshi la polisi kwa hatua hiyo..asante sana Chiba kwa kutupatia habari.

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

KATI YA KUKU NA YAI KIPI KILITANGULIA?

NGUO ZA NDANI ZINAZOBANA KWA WANAUME ZINAATHIRI UWEZO WA MBEGU ZA KIUME KUWEZA KUTUNGA MIMBA

MADHARA YA KUTUMIA DAWA ZA SILKONI KUONGEZA MAKALIO KWA WANAWAKE