KABURI LA MTOTO ALIYEFARIKI MIAKA MITATU ILIYOPITA LAFUKULIWA BAADA YA KUONEKANA YUKO HAI

comments
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida kaburi ambalo alizikwa mtoto Shabani Maulidi (15), ambaye anadaiwa kufariki dunia miaka mitatu iliyopita na kuonekana akiwa hai hivi karibuni, jana lilifukuliwa na viungo vya mwili wake kukutwa ndani.

Kazi hiyo iliyofanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi pamoja na Mtafiti wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mwanza, Lucas Ndungulu, ilizua taharuki kwa umati wa watu waliokuwa eneo hilo, baada ya nyumba ya jirani lilipo kaburi hilo, Masanja Marwa, kubomoka ghafla wakati ufukuaji huo ukiendelea, huku mwanamke mmoja ambaye hakufahamika jina lake mara moja naye akianguka na kuzirai.
Kwa sasa mtoto huyo ambaye alionekana hai, amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa uangalizi wa kitaalamu.

Akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio, Ndungulu alisema kuwa wameamua kufukua kaburi hilo ili kupata sehemu ya viungo vya mwili kwa ajili ya vipimo.

“Lengo la kufukua kaburi hili ni kutaka tupate kiungo chochote cha mwili wa marehemu ili tufanye utafiti wa kitaalamu ili tujue kama ni kweli huyu anayedaiwa kuwa ni mtoto wao ndiye,” alisema.
Alisema kuwa ufukuaji huo umemalizika na kwamba wamepata baadhi ya viungo vya mwili wa marehemu na kuchukua baadhi ya mifupa ya mapaja yote mawili ambayo itapelekwa katika hospitali ya rufaa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Kwa mujibu wa Ndugulu, majibu ya vipimo hivyo yatatolewa baada ya wiki mbili kama hakutakuwa na tatizo lolote la kukatika kwa umeme.
Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Geita, Adamu Sijaona, alisema kuwa pamoja na kuchukua viungo hivyo, pia watachukua damu ya wazazi na mtoto mwenyewe.

“Tumechukua pia damu ya mama na baba wa Maulidi mwenyewe ili tukapime vinasaba (DNA) na kama alivyosema mtafiti, majibu yatatoka baada ya wiki mbili,” alisema.

Akizungumza baada ya kazi ya ufukuaji kumalizika, baba mzazi wa mtoto huyo, Maulidi Shabani, alisema kuwa endapo majibu yatakuja tofauti au vile wanavyokusudia, wapo tayari kuyapokea na kwamba ikigundulika huyo aliyeonekana ni Maulidi, pia watampokea na kuendelea kumtunza.

“Lakini nina imani kuwa huyu aliyeonekana ni mwanangu Maulidi kabisa, kwa sababu anazo alama zote,” alisema mzazi huyo.

Mtoto Maulidi aliyefariki dunia miaka mitatu iliyopita na kufanyiwa matanga, alionekana akiwa hai baada ya kukutana na mama yake ana kwa ana mapema wiki hii asubuhi wakati akienda kwenye shughuli zake za biashara.

Ilidaiwa na wazazi wake kuwa Maulidi alitoweka ghafla na kushindwa kurudi nyumbani kwao Januari mosi 2011, wakati alipokuwa amewapeleka mbuzi malishoni na mwili wake kuonekana baada ya siku tatu akiwa amefia kwenye kisima cha maji.

Kwa mujibu wa baba yake, Maulidi hakurudi nyumbani siku hiyo, ambapo waliendelea kumtafuta bila mafanikio na ndipo baada ya siku tatu walimkuta akiwa amefia ndani ya kisima cha maji kilicho maeneo ya Kijiji cha Nyankumbu, Kitongoji cha Mwembeni.

Tukio hili ni la tatu kutokea mkoani hapa ambapo wilayani Kasamwa, mwanamke aliyefariki dunia miaka mitano iliyopita alionekana hai na kutambuliwa na ndugu yake. Tukio la pili lilitokea Wilaya ya Chato, wakati kijana aliyefariki dunia miaka miwili iliyopita alionekana akiwa hai.
CHANZO:Gazeti la Tanzania Daima

WATAKAO FELI MTIHANI WA KIDATO CHA PILI KURUDIA DARASA

comments
Wanafunzi
Wakati wanafunzi wa kidato cha pili wakitarajia kufanya mtihani wa taifa wiki ijayo, Serikali imesema watakao feli watarudia darasa hilo.Kauli hiyo imetolewa na katibu mkuu wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi profesa Sifuni Mchome alipokua akizungumza na waandishi wa habari jijini dar es salaam. Alisema jumla ya wanafunzi 531, 457 wa kidato cha pili wanatarajia kufanya mtihani huo nchi nzima.

“ watakao feli watarudia darasa hilo na watakao feli mara ya pili serikali itaangalia uwezekano wa kuwapeleka shule za ufundi au kuendelea na shule kama wanafunzi wa kujitegemea” alisema Profesa sifuni.
Alisema mtihani huo utaanza October 7 hadi 21 mwaka huu katika vituo takribani 4,437 vilivyosajiliwa kwa ajili ya kufanyia mitihani nchi nzima na wanafunzi waliojiandikisha kufanya mitihani hiyo wasichana ni 270,734 sawa na asilimia 50.1 na wavulana ni 260,723 sawa na asilimia 49.1 ambao ni sawa na ongezeko la asilimia 3.1 ikilinganishwa na watahiniwa wa mwaka jana ambao walikua 4,297.

Aidha alisema kwa upande wa makundi maalum yenye mahitaji maalumu wenye uoni hafifu ni 89 na wasiona ni 93.

JESHI LA POLISI NCHINI LIMEMFUKUZA KAZI ASKARI ALIYEINGIA UKUMBI WA DISCO AKIWA NA BUNDUKI

comments: 1
KAMANDA wa Polisi Kikosi cha Operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu na majambazi, maarufu kama Kimbunga, Simon Sirro, amesema kuwa wamemtimua askari wao aliyeingia ukumbi wa disko mjini Bukoba akiwa na bunduki kwa ajili ya kulipa kisasi.

Sirro alitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari jana wakati akielezea mafanikio waliyoyapata katika operesheni hiyo kwa kuwakamata watuhumiwa 88 wanaojihusisha na ujambazi na biashara ya silaha.
Alimtaja askari huyo kuwa ni mwenye namba H 85, PC Alphonce, aliyekuwa ametokea mkoani Mara kwa ajili ya kushiriki operesheni hiyo mkoani Kagera.

Alisema kuwa PC Alphonce alikorofishana na baadhi ya watu ndani ya ukumbi wa disko, hivyo akatoka nje kufuata bunduki, kisha akarudi nayo kwa ajili ya kuwadhuru ‘wabaya’ wake, lakini askari wenzake waliokuwamo ndani walifanikiwa kumzuia kabla ya kutimiza azima yake.

Kuhusu kukamatwa kwa Mkurugenzi wa redio ya kijamii iliyoko wilayani Karagwe (FADECCO) na kuwekwa ndani siku mbili, kisha kuachiwa kabla ya kukamatwa tena, Sirro alisema uchunguzi unaendelea kubaini uraia wake ambao umeonekana kuwa wa shaka.

Wakati huo huo, watuhumiwa 88 wa unyang’anyi wa kutumia silaha wamekamatwa wakiwamo watano wanaojihusisha na biashara ya uuzaji wa silaha mbalimbali.

Kamanda Sirro alisema kuwa wameweza kuwakamata watuhumiwa wanaojihusisha na biashara ya silaha mbalimbali kutoka nchini Burundi.

Alisema watuhumiwa hao baada ya kuhojiwa, mmoja wao alikiri kuwa alikuwa akifanya biashara ya kuuza mbuzi ambao alikuwa akiwatoa Tanzania na kuwapeleka Burundi, baadaye akashawishiwa kuwa biashara hiyo hailipi, badala yake afanye biashara ya kuuza silaha.

Kamanda Sirro aliongeza kuwa katika mahojiano hayo watuhumiwa walisema kuwa huko Burundi wanazinunua silaha kwa bei rahisi ya sh 100,000 na kuziuza kwa sh milioni 1.5 Tanzania.
Kwa mujibu wa Sirro, majina ya watuhumiwa hao yamehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi ili kuwabaini wanaozinunua huku Tanzania.

Alisema watuhumiwa wawili kazi yao ilikuwa kufuata silaha Burundi na watatu walikuwa wakizisambaza kwa wateja wao hapa nchini, na kwamba watuhumiwa wote 88 ni Watanzania.

“Silaha 23 zimekamatwa zikiwemo SMG tatu, pisto mbili, magobore 18, risasi 484 za SMG/SAR 471, pisto 13, magazine mbili za SMG, bomu moja la kutupwa kwa mkono na sare moja ya jeshi la Burundi,” alisema.
Aliongeza kuwa katika operesheni hiyo pia wamekamata ng’ombe 103 mali ya Kalemera George katika Hifadhi ya pori la Biharamulo, ambao walipelekwa mahakamani kwa kutumia sheria ya wanyamapori, ambako iliamriwa wataifishwe.

Kamanda Sirro alisema kuwa wahamiaji haramu 425 wamekamatwa katika awamu ya pili ya Opersheni Kimbunga, Wanyarwanda wakiwa 149, Warundi 180, Waganda 82 na Wakongo 14.
Wahamiaji 122 waliondoka kwa hiari na 39 waliachiwa huru baada ya mahojiano.

Alisisitiza kuwa operesheni hiyo ni endelevu na haichagui tabaka la mtu, isipokuwa inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kwa kuzingatia haki za binadamu.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima