BUSH PARTY KUFANYIKA SIKU YA PASAKA KATIKA UFUKWE WA BWALO LA POLISI MWISENGE

comments
Hawa ndio The The Track Masters DJs na Hii ilikua ni siku ya mwaka mpya tulipoangusha bonge la burudani pale bwalo la polisi mwisenge na sasa The track Masters Djs wakishirikiana na Mimi Entertainments & Promotions  tumekuandalia BUSH PARTY ni katika ufukwe wa bwalo la polisi mwisenge kutakua na burudani mbalimbali za toka kwa wasanii wa asili na wasanii mbalimbali wa shows za sebene. Kama kawaida Bonge la Disco kutoka kwa The Track Masters Djs hapa namzungumzia Dj Lima pamoja na Dj Chibarland tutafanya yetu na ww karibu ufanye yako. Burudani itaanza saa nane kamili mchana mpaka choka mwenyewe KINGILIO- Watoto 1000/= na WAKUBWA 2000/= Nyote mnakaribishwa. Imedhaminiwa na AURIC AIR, COCA COLA na POLISI MESS
Bwalo la Polisi mwisenge ndio Wadhamini wakuu wa show yetu ya BUSH PARTY siku ya pasaka kumbuka vinywaji vinapatikana kwa bei poa kabisa ya 1500 kwa vinywaji vya TBL karibuni sana kwa burudani na huduma ya vinywaji karibu na bureeeeee ukikosa hii shauri yako
Wadhamini wa kwanza wa Bush Party AURIC AIR wanasafirisha abiria kwa njia ya anga kutoka Musoma kwenda maeneo tofauti hapa nchini fika katika ofisi zao zilizopo mtaa wa ghandi au Piga simu zifuatazo kwa maelezo zaidi  +255767 11 29 28 au +255784 11 29 29 au +2557 63 11 29 29 ili upate ratiba za auric air
Coca cola pia ni wadhamini wa Tamasha la BUSH PARTY Litakalofanyika siku ya Pasaka Pale bwalo la Polisi Mwisenge coca cola watatoa zawadi mbalimbali kwa watoto na watu wazima watakaofika kusherekea nasi pale bwalo la polisi mwisenge

MISS MARA 2013 SASA KUFANYIKA MWANZONI MWA MWEZI WA SITA

comments
Mkurugenzi wa Homeland Entertainments & Promotion Bwana Godsos Mkama( Kulia) Akisisitiza kuwa Mwaka Huu lazima Mkoa wa Mara Utachukua Taji la Miss Tanzania Bila Ubishi.


Mkurugenzi wa kampuni ya Homeland Entertainments & Promotions ya Mjimi Musoma Bwana Godsos Mkama amesema shindano la Miss Mara kwa mwaka huu litafanyika wiki ya kwanza ya mwezi wa sita.

Akiongea na Chibasa Media House amesema kwa mwaka huu shindano hilo litafanyika baada ya kuwapata wawakilishi kutoka wilaya zote za mkoa wa mara ili kuingia kambini rasmi.

Amesema kuwa kwa mwaka huu amejipanga vilivyo kwa udhamini wa kampuni ya bia ya TBL atahakikisha washiriki wake wanafanya vyema kuanzia ngazi ya kanda hadi taifa.

Mkama ameongeza kuwa kwa mwaka huu shindano hilo litapambwa na wasanii wakali wa mziki wa kizazi kipya toka dar es salaam na musoma na wasanii hao wako kwenye hatua za mwisho za mazungumzo ili wasaini mkataba.

Endelea kutembelea mtandao huu ili uweze kufahamu maandalizi ya shindano hilo la miss mara 2013 na wasanii watakao kuja. 


MVUVI ANUSURIKA KULIWA NA MAMBA WILAYANI BUNDA

comments
Mamba
MVUVI, Yohana Stephano (26), mkazi wa Kijiji cha Guta wilayani Bunda mkoani Mara jana amenusurika kuliwa na mamba wakati akienda kuvua samaki maeneo ya Ziwa Victoria.

Akizungumza mara baada ya kufikishwa Kituo cha Polisi Bunda kwa ajili ya kupewa barua ya matibabu, alisema mkasa huo ulitokea majira ya saa moja asubuhi wakati akienda kuvua samaki.

Alisema siku hiyo ya tukio aliondoka asubuhi na kuchukua nyavu zake na kwenda ziwani na alipofika ziwani alikwenda sehemu ambako amekuwa akivua samaki kwa kutumia uvuvi wa miguu.

“Wakati nikiwa natandaza nyavu yangu ghafla nilishtukia nakamatwa na mamba katika mguu wa kushoto na ndipo nilipokamata majani aina ya matete huku nikipiga kelele za kuomba msaada kwa wavuvi wenzangu ambao pia walikuwa wakijiandaa kwenda kuvua samaki ziwani,”alisema.

Alifafanua kuwa baada ya mapambano yake na mamba huyo huku akipiga kelele wananchi na wavuvi wenzake waliwahi kufika kwa kutumia mitumbwi na ndipo walipofanikiwa kumuokoa.

Hata hivyo licha ya kumuokoa tayari mamba huyo alikuwa ameshamjerehi mvuvi huyo sehemu za mguu katika paja la kushoto na sehemu ya mbavu za kushoto.

Mvuvi huyo amelazwa katika hospitali ya DDH Bunda ambako anaendelea na matibabu.
Hili ni tukio la tatu tangu mwaka huu uanze kwa watu na wavuvi kukamatwa na mamba katika maeneo ya Ziwa Victoria husuan katika Kata ya Kisorya. Chanzo: Berensi Alikadi, Bunda


PROFESA SILAS RWAKABAMBA WA TANZANIA ATEULIWA KUWA WAZIRI WA MIUNDOMBINU RWANDA

comments
Rais wa Rwanda Paul Kagame
RAIS Paul Kagame wa Rwanda amemteua Mtanzania, Profesa Silas Rwakabamba kuwa Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika Jumatatu iliyopita.

Kabla ya uteuzi huo, Profesa Rwakabamba alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda. Ni mmoja wa mawaziri wanaoingiza sura mpya katika Baraza la Rais Kagame ambalo amelifanyia mabadiliko kwa kuunda wizara nyingine mpya.

Sura nyingine mpya katika Baraza hilo ambalo liliapishwa juzi Ikulu ya Rwanda ni pamoja na Seraphine Mukantabana (Wakimbizi na Menejimenti ya Maafa) na Oda Gasinzigwa (Ofisi ya Waziri Mkuu- Familia na Jinsia).

Akizungumza kwa simu na mwandishi wetu jana, mdogo wa Profesa Rwakabamba, Timothy Rwamushaija anayeishi Dar es Salaam, alisema ndugu yake alizaliwa katika Kijiji cha Bushagara, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Alisema Profesa Rwakabamba alikuwa Mtanzania aliyeamua kuchukua uraia wa Rwanda na wote baba yao ni Mzee Titus Rwamushaija... “Huyu ni kaka yangu wa tumbo moja na kwa kweli tumefurahi sana kwa mafanikio yake sisi kama wanafamilia.”

Naibu Makamu Mkuu - Taaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Profesa Makenya Maboko alisema Profesa Rwakabamba alifanya kazi katika chuo hicho na aliondoka akiwa Mkuu wa Kitivo cha Uhandisi.

“Aliondoka wakati Kagame alipoingia madarakani na alikwenda kuongoza Taasisi ya Teknolojia ya Kigali (KIST) kabla ya kwenda katika Chuo Kikuu cha Kigali,” alisema Profesa Maboko.

Msomi huyo alikwenda Rwanda mwaka 1997, baada ya kuombwa na Rais Kagame ambaye alikwenda UDSM kuwaomba baadhi ya wahadhiri kwenda Kigali kufungua chuo kikuu katika taifa lake baada ya kumalizika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994.

Profesa Rwakabamba alikuwa Mkuu wa kwanza wa KIST na kukifanya kuwa miongoni mwa vyuo bora barani Afrika kwa masuala ya teknolojia jambo lililomfurahisha Rais Kagame.

Baada ya mafanikio hayo, Rais Kagame alimteua kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda, Butare ambako pia alijizolea sifa baada ya kusimamia vyema ujenzi wa mabweni kwa wingi na kiongozi huyo alimtunukia uraia wa nchi hiyo kama zawadi.

Hata hivyo, Profesa Rwakabamba atakuwa amelazimika kuukana uraia wa Tanzania kwa kuwa katiba ya nchi hairuhusu uraia wa nchi mbili.
Profesa Rwakabamba alipata elimu ya msingi huko Muleba na akajiunga na Shule ya Sekondari ya Ihungo.

Baada ya hapo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza na kupata Shahada ya Uhandisi mwaka 1971 na 1975 alipata Shahada ya Uzamivu katika fani hiyohiyo.Chanzo Gazeti la Mwananchi.

RAIS MUGABE ATIMIZA MIAKA 89 ASEMA JUKUMU LA KUIONGOZA NI AMRI YA MWENYEZI MUNGU

comments
MUGABE
Wafuasi wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe wamekusanyika katika mji wa Bindura wenye migodi ili kusherehekea rasmi Bwana Mugabe kutimiza miaka 89.
Ripoti zinasema sherehe hiyo inagharimu dola 600,000 kutokana na mchango wa makampuni.
Wenye maduka mjini Bindura wanasema waliamrishwa kufunga maduka mapema hapo jana, ili kusaidia kusafisha mji kwa ajili ya party ya siku ya kuzaliwa ya Bwana Mugabe.

Hii ni sherehe ya pili ya Bwana Mugabe kutimiza miaka 89.
Katika party ya kwanza iliyofanywa mwezi uliopita Bwana Mugabe alisema jukumu lake la kuongoza Zimbabwe amepewa na Mungu - ni amri ya Mwenyezi Mungu.

Wapinzani wake wana wasi-wasi kuwa wafuasi wa Bwana Mugabe wanapanga kuanza tena ghasia na vitisho wakati nchi inajitayarisha kwa uchaguzi mkuu utaofanywa mwaka huu.
Wanasema tayari ofisi za makundi yanayochunguza uchaguzi zimeshambuliwa na polisi wamenyang'anya watu mamia ya redio za kuweza kusikiliza matangazo ya mbali.

Zimbabwe itafanya kura ya maoni kuhusu katiba mpya katika majuma mawili yajayo.Chanzo bbc swahili