MVUVI ANUSURIKA KULIWA NA MAMBA WILAYANI BUNDA

Mamba
MVUVI, Yohana Stephano (26), mkazi wa Kijiji cha Guta wilayani Bunda mkoani Mara jana amenusurika kuliwa na mamba wakati akienda kuvua samaki maeneo ya Ziwa Victoria.

Akizungumza mara baada ya kufikishwa Kituo cha Polisi Bunda kwa ajili ya kupewa barua ya matibabu, alisema mkasa huo ulitokea majira ya saa moja asubuhi wakati akienda kuvua samaki.

Alisema siku hiyo ya tukio aliondoka asubuhi na kuchukua nyavu zake na kwenda ziwani na alipofika ziwani alikwenda sehemu ambako amekuwa akivua samaki kwa kutumia uvuvi wa miguu.

“Wakati nikiwa natandaza nyavu yangu ghafla nilishtukia nakamatwa na mamba katika mguu wa kushoto na ndipo nilipokamata majani aina ya matete huku nikipiga kelele za kuomba msaada kwa wavuvi wenzangu ambao pia walikuwa wakijiandaa kwenda kuvua samaki ziwani,”alisema.

Alifafanua kuwa baada ya mapambano yake na mamba huyo huku akipiga kelele wananchi na wavuvi wenzake waliwahi kufika kwa kutumia mitumbwi na ndipo walipofanikiwa kumuokoa.

Hata hivyo licha ya kumuokoa tayari mamba huyo alikuwa ameshamjerehi mvuvi huyo sehemu za mguu katika paja la kushoto na sehemu ya mbavu za kushoto.

Mvuvi huyo amelazwa katika hospitali ya DDH Bunda ambako anaendelea na matibabu.
Hili ni tukio la tatu tangu mwaka huu uanze kwa watu na wavuvi kukamatwa na mamba katika maeneo ya Ziwa Victoria husuan katika Kata ya Kisorya. Chanzo: Berensi Alikadi, Bunda


Comments

Popular posts from this blog

KATI YA KUKU NA YAI KIPI KILITANGULIA?

NGUO ZA NDANI ZINAZOBANA KWA WANAUME ZINAATHIRI UWEZO WA MBEGU ZA KIUME KUWEZA KUTUNGA MIMBA

MADHARA YA KUTUMIA DAWA ZA SILKONI KUONGEZA MAKALIO KWA WANAWAKE