MBUNGE WA MUSOMA MJINI VICENTI NYERERE ASEMA BULEMBO AMEINGIZWA MJINI

VICENTI NYERERE MBUNGE WA MUSOMA MJINI
MBUNGE wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere (CHADEMA), amekana kumtambua mtu aliyejinadi alikuwa Meneja wa Kampeni wa jimbo hilo, Juma Songo, ambaye amejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kusema chama hicho kimetapeliwa.

Akizungumza na Tanzania Daima juzi, Nyerere alisema aliyekuwa meneja kampeni wake ni Fikiri Malenge, ambaye mpaka sasa ni katibu wake na wala si Songo.

Nyerere alisema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa CCM, Abdallah Bulembo, amekutana na watoto wa mjini na kumdanganya, naye akajikuta anadanganyika kama mtoto mdogo.
“Bulembo hakujua kama Musoma kuna watoto wa mjini, sasa kaingizwa chaka bovu naye kaingilika kwa kudanganywa kampeni meneja wangu alikuwa huyo Songo wakati kampeni meneja wangu ni Fikiri Malenge,” alisema.

Nyerere alisema CCM haikuwa makini katika mambo yake ndiyo maana wakapokea mtu aliyewadanganya, nao wakakubali na kuutangazia umma bila kuhakiki.

Alisema tabia ya kukurupuka kwao inawasababishia kutotimiza ahadi walizozitoa, hasa katika suala la maendeleo, ndiyo maana miradi wanayoifanya inaharibika ama kukumbwa na rushwa pamoja na ufisadi.

Aidha, alisema hofu, kuweweseka na kasi ya wananchi kuhamia CHADEMA vinawapa kiwewe ndio sababu ya kusingizia watu kuhama CHADEMA na kuingia CCM wakidhani watawatisha.

Akizungumza kwa njia ya simu akiwa njiani kuelekea jijini Mbeya, Malenge alikiri kuwa ndiye aliyekuwa kampeni meneja wa Nyerere na ndiye aliyemuwezesha kushinda nafasi ya ubunge akishirikiana na wananchi, hivyo huyo anayejinadi kwa cheo hicho ni muongo.
Malenge alisema kuwa, baada ya kumaliza kampeni alipendekezwa kuwa katibu wa Nyerere na kazi hiyo anaendelea nayo mpaka sasa.

Hivi karibuni, Bulembo alimpokea Songo ambaye alinadiwa kuwa kampeni meneja wa Nyerere, na kachero wa shughuli za usalama na uenezi mkoani Mara kupitia CHADEMA.Chanzo Tanzania Daima


Comments

Popular posts from this blog

KATI YA KUKU NA YAI KIPI KILITANGULIA?

NGUO ZA NDANI ZINAZOBANA KWA WANAUME ZINAATHIRI UWEZO WA MBEGU ZA KIUME KUWEZA KUTUNGA MIMBA

MADHARA YA KUTUMIA DAWA ZA SILKONI KUONGEZA MAKALIO KWA WANAWAKE