MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA (TCRA) YAWATOA WASIWASI WATANZANIA KUHUSU MFUMO WA DIGITALI

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imewatoa hofu wananchi wote wanaoishi katika maeneo ambayo bado kufikiwa na mfumo mpya wa mawasiliano wa digitali, akisema wataendelea kupata mawasiliano kupitia mfumo wao wa zamani wa analojia.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Meneja wa Mawasiliano wa mamlaka hiyo, Innocent Mungi wakati akifafanua kuhusu wasiwasi uliojitokeza kwa wananchi hasa walioko mikoani.
Mungi alisema watazima mtambo wa zamani kule ambako huduma hiyo mpya ya digitali imefika, kwamba kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa na mtambo huo, wataendelea kutumia televisheni zao kupitia mfumo wa zamani.

Alibainisha kuwa, hadi sasa ni asilimia 24 sawa na mikoa 11 ya nchi ndiyo itafaidika na mawasiliano hayo ya digitali, ambapo kule kusikokuwa na mawasiliano hayo bado wataendelea kupata mawasiliano kwa kutumia satelaiti, madishi na usambazaji wa nyaya hadi hapo mfumo mpya utakapowafikia.

“Naomba niwatoe hofu wananchi kuwa siyo kweli kwamba ifikapo Desemba 31, serikali itazima mitambo ya analogia nchi nzima, hiyo haiwezekani na wala siyo rahisi kufikisha huduma ya digitali kwa mara moja katika maeneo yote ya nchi,” alisema.

Alitoa wito kwa wananchi kuwa wasikubali kudanganyika na maneno ya mitaani kuwa ‘televisheni za kichogo’ mara ifikapo mwishoni mwa mwezi huu hazitatumika tena.

Mungi alisema maeneo yote ambayo yamefungwa mtambo huo wa digitali wasitupe televisheni zao kwani zitaendelea kutumika ilimradi wanunue king’amuzi.
Alisema mfumo huo mpya utaleta mapinduzi makubwa katika mawasiliano, zikiwemo faida kama vile huduma zote zilizokuwa zikifanyika katika simu za viganjani.Chanzo Tanzania Daima

Comments

Popular posts from this blog

KATI YA KUKU NA YAI KIPI KILITANGULIA?

NGUO ZA NDANI ZINAZOBANA KWA WANAUME ZINAATHIRI UWEZO WA MBEGU ZA KIUME KUWEZA KUTUNGA MIMBA

MADHARA YA KUTUMIA DAWA ZA SILKONI KUONGEZA MAKALIO KWA WANAWAKE