KIPIMO CHA X-RAY KATIKA HOSPITALI YA MKOA WA MARA KIMEFANYIWA MATENGENEZO
MGANGA MFAWIDHI WA HOSPITALI YA MKOA WA MARA IRAGI NGERAGEZA AKITOA MAELEZO KWA BAADHI YA WAANDISHI WA HABARI. |
Baadhi ya wagonjwa wanaokwenda hospitali ya Mkoa wa Mara
kupima kipimo cha X-ray wamelalamikia uongozi wa hospitali hiyo kutotoa taarifa
kwa wagonjwa baada ya kukosekana kwa huduma hiyo kwa muda.
Wakiongea na gazeti hili leo wakiwa nje ya chumba cha x-ray
mmoja wa wagonjwa Bi Mage Hilary amesema toka siku ya jumatatu amekuwa akiwahi
kila siku asubuhi ili kupata huduma hiyo lakini ameshindwa kuipata na hakuna
taarifa yoyote toka kwa daktari kwa nini hataki kuwahudumia.
“Ndugu mwandishi hii sio haki kabisa we fikiria toka asubuhi
tuko hapa na hakuna taarifa yoyote toka kwa daktari kwanini huduma haitolewi
tunawaona tu madaktari wanapita hapa wanatuona kama majengo je hii ni haki
kweli” alisema bi Mage.
Naye Piter Majaliwa mkazi wa kigera manispaa ya musoma amesema
kuwa kwa muda wa wiki moja amekuwa akifika hospitalini hapo kupata huduma hiyo
baada ya kupata ajali ya pikipiki na kuumia ubavu wa kushoto lakini kila
anapofika hapati huduma na hivyo anashindwa kuelewa tatizo ni nini kwani hakuna
taarifa iliyotolewa kwao ili wajue nini cha kufanya.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini
kuwa huduma ya x-ray katika hospitali hiyo ilikuwa haipatikani kwa muda wa wiki
mbili kutokana na mashine kuharibika ghafla.
Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Iragi Ngerageza amesema
kuwa mashine ya x-ray iliharibika ghafla wiki mbili zilizopita na walikuwa
wanawasubiri mafundi kutoka kampuni ya Philips ambayo ndio walipewa tenda ya
kufunga na kutengeneza mashine hiyo.
Amesema baada ya tatizo hilo kutokea walishindwa kuchukua
mafundi sehemu nyingine kwa ajili ya kuitengeneza kwani tayari walishaweka
makubaliano na kampuni ya Philips kuwa wao ndio watakua wanaifanyia matengenezo
mashine hiyo, na kilichosababisha mashine hiyo kuharibika ni kutofanyiwa
matengenezo kwa muda mrefu.
Ameongeza kuwa uongozi wa hospitali hiyo umejitahidi
kulishughulikia tatizo hilo na tayari wamefanikiwa kurejesha huduma hiyo lakini
changamoto inayowabili pia ni uchache wa madakitari na wauguzi katika kutoa
hudumia.
Aidha amesema kuwa changamoto nyingine inayowakabili ni
fedha ambapo ili hospitali iweze kuendesha shuguli zake kwa ufasaha inahitaji
shilingi milioni ishirini na sita(26) kwa mwezi lakini wamekuwa wakishindwa
kufikia lengo hilo kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na swala la
rushwa lakini kwa sasa wanatarajia kufikisha lengo la kukusanya kiasi hicho cha
pesa ama zaidi baada ya kufanya kazi na watu kutoka taasisi ya kupambana na
kuzuia rushwa takukuru.
Comments
Post a Comment