MBUNGE WA VITI MAALUMU ESTER BULAYA (CCM) AMEITAKA SERIKALI KUONDOA URASIMU ILI KUTOA HABARI KWA MUDA UNAOTAKIWA KWA WANAHABARI WANAPOZIHITAJI

Bungeni Dodoma
MBUNGE wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM), jana aliitaka serikali kuondoa urasimu ili iweze kutoa habari kwa wakati na muda unaotakiwa pindi wanahabari wanapozihitaji.

Bulaya alitoa kauli hiyo jana bungeni alipouliza swali la nyongeza ambapo alisema kuwa kumekuwa na ukiritimba wa utoaji wa habari kwa taasisi za serikali hali inayosababisha upatikanaji wa habari kuwa ni mgumu.

“Mheshimiwa Spika, serikali imekuwa na ukiritimba mkubwa kwa taasisi zake kutoa habari kwa waandishi pale wanapohitaji, ingawa ni haki yao lakini wanazungushwa na kusababisha habari zinaandikwa upande mmoja, naomba serikali ituambie ni kwa nini hawatoi habari?” alihoji Bulaya.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Tumbe Rashid Ali Abdallah (Cuf) alitaka kujua ni waandishi wangapi wanamaliza mafunzo yao kila mwaka.

Mbunge huyo pia alihoji ni waandishi wangapi wanaoajiriwa na serikali na wangapi wameajiriwa na serikali na hatimaye kuacha kazi.

Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Amos Makala alisema hadi sasa Tanzania inavyo vyuo vinavyofundisha taaluma ya habari na Mawasiliano ambavyo vinatambulika na Baraza la Taifa la Ufundi vipatavyo vinane.

Alisema katika vyuo hivyo, vipo vyuo vikuu vinne ambavyo vinatoa taaluma hiyo na vyuo vingine vinatoa taaluma hiyo kwa ngazi ya cheti.

Kuhusu idadi ya wanafunzi wanaomaliza vyuo vya habari na mawasiliano kila mwaka nchini ni kubwa ingawa idadi ya wanaoajiliwa ni ndogo.

“Mathalani, katika shule kuu za uandishi wa habari na mawasiliano ya umma wastani wa wanafunzi mia moja wanamaliza masomo na kutunukiwa shahada na stashahada zao kila mwaka kuanzia miaka ya 2002/2003 hadi 2011/12,” alisema Makala.

Alisema serikali imeajiri waandishi wa habari zaidi ya mia tatu wanaofanya kazi kama maofisa habari na mawasiliano katika wizara, idara zinazojitegemea, mamlaka, wakala na taasisi mbalimbali za serikali.
Alibainisha kuwa idadi ya waandishi wa habari ambao wameajiriwa na serikali na hatimaye wakaacha kazi serikalini bado ni ndogo.

Akizungumzia ukiritimba wa utoaji habari katika taasisi za serikali, waziri alisema tayari wito ulishatolewa kwa watumishi wote kutoa habari kama zinavyotakiwa kwa kuwa ni haki ya waandishi kuzipata.
chanzo: Tanzania Daima

Comments

Popular posts from this blog

KATI YA KUKU NA YAI KIPI KILITANGULIA?

NGUO ZA NDANI ZINAZOBANA KWA WANAUME ZINAATHIRI UWEZO WA MBEGU ZA KIUME KUWEZA KUTUNGA MIMBA

MADHARA YA KUTUMIA DAWA ZA SILKONI KUONGEZA MAKALIO KWA WANAWAKE