JOHN MNYIKA ATOA WITO KWA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KUTOA RASIMU YA SERA YA GESI ASILIA KWA LUGHA YA KIINGEREZA NA KISWAHILI

Mbuge wa Ubungo John Mnyika
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), amepingana na hatua ya Wizara ya Nishati na Madini kutoa rasimu ya sera ya gesi asilia kwa Lugha ya Kiingereza pekee na kutoa wito sera hiyo kuandikwa pia katika lugha ya Kiswahili.

Mnyika alisema hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana na kumtaka Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Sospeter Muhongo, kuutangazia umma kwamba, rasimu hiyo itatolewa pia kwa lugha ya Kiswahili na kwamba, ichapwe katika vyombo vingine vya habari.

“Izingatiwe kuwa napinga hatua ya Wizara ya Nishati na Madini kuchapa rasimu ya Sera ya Taifa ya Gesi Asili kwa Lugha ya Kiingereza pekee kwenye baadhi ya magazeti tarehe 2 Novemba 2012, huku Katibu Mkuu wa Wizara hiyo akitoa mwito kwa wadau na Watanzania wote kutoa maoni hali, ambayo itakuwa ni kikwazo kwao kushiriki katika mchakato wa maandalizi ya sera yenye kuzingatia maslahi ya taifa,” alisema Mnyika katika taarifa hiyo.

Alisema kitendo cha Bodi mpya ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kusogeza mbele muda wa kukamilisha ripoti yao kutoka Septemba 30 hadi Novemba 30, mwaka huu, kutakosesha nafasi ya kutoa maoni ya kuboresha rasimu hiyo ya sera kwa madai kwamba, matokeo ya mapitio hayo yanafanyika kwa kutumia fedha za umma.

Alimtaka Waziri Muhongo kutumia fursa hiyo kuweka hadharani matokeo ya agizo lake la kupitiwa upya kwa mikataba yote 26 ya utafutaji mafuta na gesi asili ili udhaifu uliobainika kwenye mikataba hiyo utumiwe na umma kutoa maoni na mapendekezo ya kuboresha sera, sheria, taasisi na mfumo mzima wa uingiaji wa mikataba.

Mnyika, ambaye pia ni Waziri Kivuli katika Wizara ya Nishati na Madini, alimtaka Waziri Muhongo kueleza namna kamati mbalimbali za kudumu za Bunge zitakavyohusishwa katika mchakato wa kukusanya maoni pamoja na kuishauri na kuisimamia serikali kutokana na unyeti wa sera hiyo.

Chanzo:ipp media

Comments

Popular posts from this blog

KATI YA KUKU NA YAI KIPI KILITANGULIA?

NGUO ZA NDANI ZINAZOBANA KWA WANAUME ZINAATHIRI UWEZO WA MBEGU ZA KIUME KUWEZA KUTUNGA MIMBA

MADHARA YA KUTUMIA DAWA ZA SILKONI KUONGEZA MAKALIO KWA WANAWAKE