CHADEMA YATAKA MFUMO WA SHERIA KUSIMAMIA MABADILIKO

Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema wakati umefika kwa nchi kuwa na mfumo wa kikatiba na sheria kwa ajili ya kusimamia mabadiliko kufanyika kwa amani ili kuepusha nchi kuingia katika vurugu na mkanganyiko wa kisiasa.

Mbowe alisema hayo jana wakati akizungumza na wananchi kwenye mikutano ya kampeni ya uchaguzi mdogo kata za Mpapa, wilayani Momba na Myovizi, Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya.

Mbowe alisema ingawa utaratibu huo unaweza kuonekana kuwa ni dhana mpya kutokana na umuhimu wake kwa ajili ya mustakabali mwema wa Taifa, ni vyema Watanzania wakaanza kuitafakari kisha wadai kuwepo kwa mfumo huo wa kikatiba na sheria.

Alitoa mfano nchi ya Ghana ilipitia katika misukosuko ya kisisasa kutoka utawala wa Jerry Lawrings kwenda kwa Kuffour wa chama cha NPP.

“Wenzetu wale walijifunza, walipoingia madarakani wakaamua kutunga sheria ya kusimamia ‘transition period’ kutoka uongozi wa serikali moja kwenda nyingine,” alisema Mbowe.

Alisema Watanzania wanaweza kujiuliza kwa nini Marekani inachukua siku 72 kwa Rais kuapishwa na kukabidhiwa rasmi mamlaka ya kuongoza nchi, tangu achaguliwe ni kwa sababu kuna vitu  muhimu sana vya  kusimamiwa na kufanyiwa kazi kabla utawala mpya haujakabidhiwa Ikulu.

Alisema ni hatari kwa nchi kama Tanzania ambayo sasa inapitia kwenye wimbi kubwa la mabadiliko ya kisiasa, kukosa mfumo huo wa kuhakikisha mabadiliko ya mpito kutoka utawala wa serikali moja kwenda nyingine yanafanyika kwa amani na kulinda maslahi ya nchi bila vurugu.

“Ni muhimu kuwa na sheria itakayohakikisha ‘transition’ ya kutoka serikali ya chama fulani kwenda chama kingine au serikali moja kwenda serikali nyingine, kufanyika kwa amani na kwa kuhakikisha maslahi ya umma na nchi yanazingatiwa,” alisema.

 Aliongeza kuwa hapa nchini kuna mfano mzuri wa madhara ya kukosekana kwa sheria hiyo ya kusimamia kipindi cha mpito na kwamba wizi mkubwa wa kashfa ya wizi uliofanyika Benki Kuu kabla Rais aliyechaguliwa hajaapishwa na watu walitumia fursa hiyo mabilioni ya fedha katika benki hiyo.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, alikumbushia namna ambavyo sehemu ya mabilioni ya ufisadi wa fedha za malipo ya madeni ya Nje (EPA) yalihamishwa Desemba 31, 2010.



Chanzo: IPP MEDIA


Comments

Popular posts from this blog

KATI YA KUKU NA YAI KIPI KILITANGULIA?

NGUO ZA NDANI ZINAZOBANA KWA WANAUME ZINAATHIRI UWEZO WA MBEGU ZA KIUME KUWEZA KUTUNGA MIMBA

MADHARA YA KUTUMIA DAWA ZA SILKONI KUONGEZA MAKALIO KWA WANAWAKE