BoT yaipandisha hadhi benki ya DCB

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeitunuku benki ya DCB leseni ya kuipandisha hadhi kuwa ya kibaiashara hivyo kuipa fursa ya kuhudumia wafanyabiashara wadogo na wakubwa nchi nzima.

Kabla ya kutunukiwa hadhi hiyo jana, DCB ilikuwa ikihudumia wafanyabiashara wadogo wadogo wa mkoa wa Dar es Salaam tu.

"Leo hii napenda kuujulisha umma wa Tanzania kuwa BOT imetoa rasmi leseni mpya kwa benki hii (DCB) na hivyo kuifanya rasmi kuwa benki ya biashara," alisema Balozi Paul Rupia, Mwenyekiti wa Bodi ya DCB, wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana.

Kutokana na hatua hiyo, Rupia alisema kwa sasa wanajiandaa na mchakato wa kufungua matawi nchi nzima.

Pamoja na kupandishwa hadhi, Rupia aliwatoa wasiwasi wajasiriamali kuwa wasihofu kuwa DCB itawatupa bali imeongeza nguvu ya kuweza kuwahudumia.

"Dira na dhima ya benki hii itakuwa ni ile ile, zaidi itaongeza wigo mkubwa kwa wateja wetu Tanzania nzima," alisema Balozi Rupia.

Alisema DCB ilianzishwa mwaka 2002 ikiwa na lengo la kusaidia wafanyabiashara wadogo wa Dar es Salaam lakini baada ya kufanya vizuri kazi hiyo kwa weledi mkubwa, na mtaji wake umekua hadi kufikia Sh15 bilioni.

Katika kipindi cha mwaka uliopita, alisema benki hiyo yenye matawi matano Dar es Salaam, ilipata faida ya Sh2 na sasa wana mpango wa kujiandaa kuingia katika soko la hisa.
Ili kuendelea kufanikisha mafanikio ya benki hiyo, Balozi Rupia alizitaka taasisi za Serikali mikoani kama vile Halmashauri kuitumia benki hiyo ambayo inayoongozwa na wazawa nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Edmund Mkwawa alisema lengo lao ni kuhakikisha wanauza hisa na kupandisha mtaji wao hadi kufikia Sh30 bilioni.




Chanzo: Gazeti la Mwananchi

Comments

Popular posts from this blog

KATI YA KUKU NA YAI KIPI KILITANGULIA?

Timu ya wachezaji watumishi wa manispaa ya musoma ipo njia panda kwenda kushiriki katika mashindano ya shirikisho la michezo serikali za mitaa Tanzania Shimisemta

TOZI GAMBA AFUNIKA SHOW YAKE NA THE TRACK MASTERS DJS BWALO LA POLISI MWISENGE SIKU YA CHRISTMAS