Fahamu Jinsi Wavuvi wa Mwalo wa Kayenze Ndogo ilemela Mwanza Wanavyotumia Solar Kukausha Dagaa Kwa Kutumia Solar Dryer
Na Emmanuel Chibasa
Katika mwalo wa Kayenze ndogo, wilaya ya Ilemela, jijini Mwanza, wavuvi na wafanyabiashara wa dagaa sasa wanashuhudia mabadiliko makubwa kupitia teknolojia ya kisasa ya nishati ya jua, inayotumika kukausha dagaa. Mradi huu, unaoendeshwa na kampuni ya Millennium Engineers, umeleta matumaini mapya kwa sekta ya uvuvi kwa kuwawezesha wavuvi kukausha dagaa kwa ubora unaokidhi viwango vya soko la ndani na nje ya nchi.
Kwa Nini Teknolojia Hii ni Muhimu?
Teknolojia mpya ya ukaushaji dagaa kwa kutumia mitambo ya nishati ya jua ni muhimu kutokana na kutajwa kuwa suluhisho la kukabiliana na changamoto ya upotevu na uchakataji wa dagaa zenye ubora na hivyo kuongeza tija kwa wavuvi na wachuuzi katika ziwa victoria.
Wavuvi na wafanyabiashara ya dagaa wanasema, Kabla ya mradi huo, wailikua wakianika dagaa kwenye mchanga au kwenye vichanja vya miti kando ya ziwa Victoria na njia hizi za jadi zilikuwa na changamoto kadhaa, zikiwemo kuathiri usafi wa dagaa, kuvutia uchafu na wadudu, na kusababisha upotevu wa dagaa kutokana na hali ya hewa isiyotabirika. Teknolojia ya nishati ya jua imebadilisha hali hiyo kwa kuwezesha dagaa kukauka kwa usafi na haraka, na hivyo kuongeza thamani ya bidhaa.
Agness Selestine ni mmoja wa wafanyabiashara wa dagaa, amesema ukaushaji kwa kutumia nishati ya jua umewapunguzia changamoto nyingi, hasa wakati wa mvua.
“Dagaa sasa zinakauka haraka na zikiwa safi zaidi, tofauti na ilivyokuwa kwa kukausha kwenye mchanga."Naye Latifa Buchoji kwa upande wake anasema teknolojia hiyo mpya imewapa uhakika wa ubora wa dagaa, ambao unakubalika zaidi kwenye masoko hata ya nje hivyo ni mkombozi kwa biashara yao.
Madhara ya Kunianika Dagaa kwenye Mchanga
Dagaa, ni chakula maarufu duniani na wanatajwa kuwa na faida nyingi katika mwili wa binadamu ikiwa ni pamoja na kuongeza faida kwa chakula cha usawa, kwa kuwa ni chini ya mafuta yaliyojaa na kalori, lakini juu ya protini. Pia hutoa safu nzuri ya vitamini na madini lakini wataalam wa lishe wanasema kuna madhara kadhaa kwa binadamu endapo dagaa wataanikwa katika mchanga na sehemu isiyo salama ambayo ni pamoja na;
Hatari ya Uchafuzi: Kuwaanika dagaa moja kwa moja kwenye mchanga huwafanya wachafuke na kupata vumbi, bakteria, na uchafu mwingine ambao unaweza kusababisha magonjwa ya njia ya chakula.
Vimelea vya Magonjwa: Mchanga una bakteria na vimelea vinavyoweza kusababisha maambukizi ya magonjwa kama vile kuhara, kipindupindu, na magonjwa mengine ya tumbo. Dagaa walioanikwa chini wanaweza kuwa na vimelea hawa hatari kwa afya.
Sumu na Kemikali: Mchanga unaweza kuwa na sumu au kemikali kutoka kwenye mazingira yanayozunguka, ambazo zinaweza kupenya kwenye dagaa. Hii inahatarisha afya kwa muda mrefu iwapo dagaa walio na sumu hizi wataliwa mara kwa mara.
Ubora wa Chini wa Lishe: Dagaa walioanikwa chini wanaweza kupoteza baadhi ya virutubisho muhimu kutokana na kuathirika na vumbi na jua kali moja kwa moja, hivyo kupunguza thamani ya lishe ya dagaa hao.
Harufu na Ladha Mbaya: Dagaa walioanikwa kwenye mchanga wanaweza kupata harufu na ladha ya vumbi, hali ambayo inawafanya wasiwe na ladha nzuri na kuvutia kwa walaji.
Jinsi Mradi Huu Unavyofanya Kazi
Kwa mujibu wa mtaalamu wa nishati ya jua kutoka Millennium Engineers Mhandisi Wistone Nnko anesema kabla ya kuanzisha mradi huo wafanya biashara na wavuvi walikua wanaanika dagaa katika mchanga au katika vichanja na walikua wakitumia muda mrefu katika kazi hiyo.
“Mradi wetu umekuja kuleta mapinduzi katika sekta ya uvuvi ziwa Victoria, ambapo wavuvi walikua wanakabiliwa na changamoto mbambali ikiwa ni pamoja nyenzo za uvuvi wakati wa usiku walikua wanatumia karabai ambazo sio rafiki kwa mazingira, lakini pia katika eneo la ukaushaji, ambapo walikua wanafanya kazi katika eneo ambalo sio salama na walikua wanatumia masaa nane hadi kumi kwa siku.
Tumeleta teknolojia ya kisasa yanayotumia solar kukausha dagaa, ambapo wakina mama baada ya kununua dagaa kwa wavuvi wanaleta hapa kiwandani, wakileta tunazipima na kuzifanyia usafi kisha tunaanza na kuziweka kwenye dryer ambayo inatumia masaa matatu tu kukausha dagaa, mradi wetu umekuja kuongeza ubora wa mazao ambayo yanatokana na dagaa na kufikia vigezo vya kimataifa ili watu wanaofanya kazi kwenye hii sekta wanufaike na wanachokifanya” Amesema Mhandisi Wistone
Uwekezaji katika Taa za Sola kwa Mavuno Bora
Mbali na kukausha dagaa, mradi huu pia unalenga kuzalisha na kusambaza taa za sola zenye mwanga wa kutosha kwa ajili ya shughuli za uvuvi. Taa hizi zinaweza kuchochea mavuno bora kwa wavuvi wa dagaa na hivyo kusaidia kuboresha maisha yao.
Frank Faustine ni miongoni mwa wavuvi katika mwalo wa Kayenze Ndogo anasema tangu ameanza kutumia taa za solar amekua akivua dagaa wengi tofauti na alivyokua anatumia taa za karabai huku Mhandi Wistone akieleza jinsi teknolojia hiyo inavyoweza kusaidia wavuvi kutatua changamoto katika mialo tofauti ndani ya ziwa Victoria pamoja na kuwasaidia wafanyabiashara na wavuvi kutafuta masoko ya kimataifa ili waweze kupata faida zaidi.
"Taa za sola zinatoa mwanga wa kutosha unaosaidia kuvutia dagaa kwa wingi na kuokoa gharama za mafuta. Pia, zinatusaidia kuepuka uchafuzi wa mazingira unaotokana na matumizi ya taa za karabai na betri za asidi, ambazo ni hatari kwa viumbe hai," amesema Frank.
Changamoto Zinazowakabili Wavuvi wa Dagaa
Licha ya mafanikio haya, bado kuna changamoto katika mialo mingine ya Ziwa Victoria kama vile mwalo wa Busekera huko Musoma Vijijini na mwalo wa Makoko wilaya ya Musoma Mjini. Katika maeneo haya, wavuvi bado hutegemea kukausha dagaa kwa njia za jadi kwa kutumia mchanga au vichanja, hali inayosababisha hasara kubwa kutokana na uchafu na hali ya hewa isiyotabirika. Ukosefu wa teknolojia hii husababisha dagaa kushindwa kufikia viwango vya usafi vinavyohitajika kwenye soko la kimataifa, hivyo kuathiri biashara.
Faida za Kuendeleza Teknolojia Katika Maeneo Mengine
Ni dhahiri kuwa uwekezaji katika teknolojia ya nishati ya jua unaweza kuboresha hali ya mialo mingine kama Busekera wilaya ya musoma vijijini na Makoko uliopo katika manispaa ya Musoma. Kwa kutumia teknolojia hii, wavuvi wataweza kuboresha ubora wa bidhaa zao, kupunguza upotevu wa dagaa, na kuongeza thamani ya biashara zao, hivyo kufikia masoko ya kitaifa na kimataifa kwa urahisi zaidi.
Wito kwa Serikali na Wadau wa Maendeleo
Mafanikio ya teknolojia hii yanaonyesha kuwa uwekezaji katika nishati safi na rafiki kwa mazingira una umuhimu mkubwa katika sekta ya uvuvi. Mhandisi Wistone Nnko anatoa wito kwa serikali kutoa ruzuku ili kurahisisha upatikanaji wa vifaa vya nishati ya umeme jua kwa gharama nafuu kwa wavuvu na wafanyabiashara katika sekta ya uvuvi.
“Naamini kwamba serikali ina malengo mazuri sana kwa sasa na baadae, teknolojia hizi ambazo zinakuja kutatua changamoto katika sekta ya uvuvi naiomba serikali itoe ruzuku ili tunaponunua vifaa kutoka nje ya nchi visitozwe kodi pale bandarini kwa kufanya hivyo tutavipata kwa bei ambayo ni rafiki lakini pia sisi pia tutakapo vipeleka kwa walengwa wa mwisho pia watavipata kwa gharama ambayo ni nafuu.
Tunatoa mwito kwa makampuni, taasisi za maendeleo, na serikali kuwekeza katika miradi kama hii ili kuwasaidia wavuvi wa dagaa wa Ziwa Victoria kufaidika na rasilimali za ziwa kwa njia endelevu.
Aidha, Sekta inatoa ajira kwa watanzania zaidi ya milioni 6.0 pamoja na ajira za moja kwa moja kwa wavuvi 198,475 na wakuzaji viumbe maji 35,986. Uzalishaji uliofanywa na waajiriwa hawa umewezesha familia kupata kipato pamoja na kuongeza usalama wa chakula na lishe ambapo Sekta huchangia 46 asilimia 30 ya protini inayotokana na wanyama. Pia,inakadiriwa kwamba, kwa wastani, kila mtanzania anakula kiasi cha kilo 7.9 kwa mtu kwa mwaka.
Comments
Post a Comment